29th March 2020

Mamia waamshana pwani kunywa chai rangi ili kuzuia corona

Estimated reading time: 7 minute(s)

Kumetokea kisa cha kushangaza majogoo ya Jumapili, Machi 29, baada ya uvumi kuwa dawa ya virusi vya korona imepatikana.

Simu nyingi zilipigwa na jumbe za sms kutumwa huku watu wakiamshana kaunti za pwani, Kenya, eti dawa dhidi ya virusi hivyo ni chai rangi isosukari.

Watu walitakiwa kuchemsha maji na kutia majani na kisha kunywa bila kiteremshio chochote kuanzia saa nane usiku na kabla ya saa kumi na mbili asubuhi.

Uvumi ulienea kuwa, haya yote yalibainika na mtoto aliyezaliwa kwenye hospitali ya Coast General – Mombasa usiku huo huo, akatoa habari hizo, na kisha akafa.

Ndugu zetu wa kiislamu walitakiwa pia waswali wakati huo.

Kulingana na wakenya wengi toka Kwale, Kilifi n Mombasa waliopokea habari hizo, walitii na kutayarisha chai rangi ili tu kujaribu bahati yao na kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ambao umetikisa dunia na kuua watu zaidi ya elfu tano na kuambukiza zaidi ya elfu nane duniani.

****Mimi ninayeandika habari ino, pia nilipokea simu kutoka kwa mpenzi wangu, kwa mapenzi aliyonayo kwangu kuwa nisiachwe nyuma ila nipate kujikinga na virusi hivyo. (Ahsante sana mpenzi wangu, Yarrabi akulinde)****

Kenya, kufikia Machi 28, maambukizi yalikua 38, huku mmoja akiaga dunia. Kilifi ni kaunti ya pwani inayoongoza na visa 6, Mombasa 2, Kwale 1, kaunti ya Kajiado 1 ilhali Nairobi yaongoza na visa 28.

Amerika, Italia na Uchina ndizo nchi zilizoathirika zaidi.

Kwenye mitandao ya kijamii, haswa Facebook na WhatsApp, habari za uvumi huu ulienea huku wengine wakianzisha mzaha kwenye suala hilo.

Aki’comment’ juu ya uvumi huo, Mbunge mwakilishi wa akina mama kaunti ya Kwale, Zuleikha Juma Hassan alisema naye pia alipokea simu.

“Nani kati yenu ameamka usiku kupika na kunywa chai ya rangi leo? Nimepigiwa simu kadhaa leo usiku kuambiwa niamke nipike chai ya rangi ninywe. Nimeambiwa kuna mtoto amezaliwa Coast General Hospital amesema, “watu wote waamke wanywe chai ya rangi wakati fulani, ili ugonjwa wa Corona upotee”.

Hata hivyo, Zuleikha alisema hizo zote ni fununu tupu na wengi wameingiwa tu na wasiwasi juu ya ugonjwa huo.

“Mwenyezi Mungu atuepushie maradhi ya wasi wasi wakati huu wa mtihani wa virusi vya Corona,” aliongeza mbunge huyo.

Kulingana na shirika la afya duniani, WHO,  wataalamu wapo mbioni kutafuta kinga dhidi ya virusi vya korona ila kufikia sasa, hakujapatikana dawa ya virusi hivyo vilivyotokea Uchina, mwezi Desemba, 2019.

Hits: 2187
Follow, like us on social media..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Translate »
Contact VashMedia for right click rights or subscribe!